FASIHI


Fasihi ni sanaa ya lugha. Fasihi hutumia lugha kutoa sanaa mbalimbali katika jamii.

Kuna tanzu mbili kuu za fasihi, na kila utanzu una vipera vyake:
  1. Fasihi Simulizi
    1. Hadithi (Ngano) - hekaya, mighani, visasili n.k
    2. Nyimbo - za jandoni, za ndoa, za kazi n.k
    3. Maigizo - michezo ya kuigiza, ngomezi n.k
    4. Tungo Fupi - methali, vitendawili n.k

  2. Fasihi Andishi
    1. Hadithi Fupi - hadithi isiyokuwa ndefu iliyochapishwa katika mkusanyiko wa hadithi nyingine
    2. Riwaya - hadithi ndefu iliyochapishwa katika kitabu chake pekee
    3. Tamthilia - mchezo wa kuigiza uliowekwa kwa maandishi
    4. Ushairi* - mashairi yaliyoandikwa


Tofauti kuu kati ya fasihi simulizi na fasihi andishi ni kwamba Fasihi Simulizi huwasilishwa kwa njia ya mdomo au matendo ilhali Fasihi Andishi huwasilishwa kwa njia ya maandishi.
  • Tanbihi:Ushairi ni kipera cha nyimbo lakini pia mashairi yanaweza kuwa chini ya Fasihi Andishi, ikiwa yamechapishwa.


  • Tofauti kati ya Fasihi Andishi na Fasihi Simulizi


  • FASIHI SIMULIZIFASIHI ANDISHI
    1.Huwasilishwa kwa njia ya mdomo na/au matendo.Huwasilishwa kwa njia ya maandishi
    2.Ni mali ya jamii.Kazi andishi ni mali ya mwandishi (na mchapishaji)
    3.Msimulizi anaweza kubadilisha sehemu fulaniKitabu kilichoandikwa hakiwezi kubadilishwa
    4.Huhifadhiwa akiliniHuhifadhiwa vitabuni
    5.Kazi simulizi hubadilika na wakatiKazi andishi haibadiliki na wakati
    6.Huhitaji msimulizi na hadhira yake wawe mahali pamoja wakati wa masimuliziMsomaji anaweza kusoma kitabu cha hadithi peke yake, mahali popote, wakati wowote
    7.Mtu yeyote anaweza kutunga na kusimuliaNi lazima mwandishi na msomaji wawe na uwezo wa kusoma
    8.Hutumia wahusika changamano (wanyama, watu, mazimwi n.k)Hutumia wahusika wanadamu.


  • Umuhimu wa Fasihi Katika Jamii


    • Kuburudisha jamii. Takribani vipera vyote vya fasihi huwa na kusudi la kufurahisha, kutumbuiza na kusisimua hadhira.
    • Kuelimisha. Fasihi hukusudia kuelimisha hadhira kuhusu jamii, mazingira n.k
    • Kudumisha maadili katika jamii kwa kuelekeza, kuonya na kunasihi hadhira jinsi ya kufuata mwelekeo unaokubalika katika jamii.
    • Kuunganisha jamii. Fasihi huleta pamoja watu katika jamii. Kwa mfano, katika nyimbo, miviga, vichekesho.
    • Kukuza lugha. Aghalabu tungo zote za fasihi hutumia lugha. Isitoshe, fasihi hutumia mbinu nyingi za lugha. Wasimulizi na waandishi wa fasihi huhitaji kuwa na ukwasi wa lugha.
    • Kuhifadhi mila, tamaduni na itikadi za jamii. Aghalabu kazi za fasihi (hasahasa Fasihi Simulizi) huambatanishwa na desturi mbalimbali za jamii husika.
    • Kukuza uwezo wa kufikiri. Vipera vingi vya fasihi huwachochea hadhira kufikiri sana ili kupata suluhisho. k.m vitendawili, ngano za mtanziko n.k

  • No comments:

    Post a Comment